na Mwanja Ibadi, Lindi
VIONGOZI na watendaji wapatao 50 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Lindi Mjini, wamesimamishwa kazi kwa madai ya kukisaliti chama chao.
Habari za uhakika kutoka ndani ya chama hicho, ambazo zimelifikia Tanzania Daima, zinasema wanachama hao wamesimamishwa kazi kuanzia Oktoba 24 mwaka huu.
Kwa mujibu wa barua walizokabidhiwa watendaji hao, wakiwemo makatibu wa kata, matawi na wenyeviti wa serikali za mitaa katika Manispaa ya Lindi Mjini, zinazodaiwa kusainiwa na Katibu wa Chama hicho, Wilaya ya Lindi Mjini, Zainabu Chinowa, zinaonyesha wamesimamishwa uongozi kwa muda usiojulikana.
Baadhi ya barua hizo ambazo nakala zake zimepelekwa kwa katibu wa chama hicho ngazi ya mkoa na wenyeviti wa CCM ngazi za kata na Tanzania Daima, kupata nakala zake zinabainisha kuwa ukomo wa kusimamishwa kwao kutategemea na uamuzi wa kikao cha kamati ya siasa cha wilaya kitakapokutana.
Watendaji hao walisema barua hizo wamekabidhiwa na wamekabidhiwa na Katibu Mwenezi wa chama hicho, Abdallah Hamisi Livembe, ambapo barua hizo ziliwataka wakabidhi mali za chama kwa ngazi husika wakati taratibu nyingine zikiendelea.
Wakizungumza kwa niaba ya wenzao kwa masharti ya kutotajwa kwa majina yao, watendaji hao walisema kuwa wanahisi sababu za kusimamishwa kwao ni msimamo wao wa kutokuwa tayari kuvunja makundi yaliyopo ndani ya chama hicho ambayo kwa kiasi kikubwa yalichangiwa na mchakato wa kura za maoni.
“Kusimamishwa kwetu kunadaiwa sisi ni watu wa kundi la Bakari Maguo, ambaye alishindwa kwenye kura za maoni kwa mizengwe lakini tulitakiwa kuvunja makundi kwa ajili ya kumuunga mkono Mohamedi Abdullaziz, sisi tuligoma kufanya hivyo kwa kuwa si wanafiki,” walisema.
Walisema kuwa sababu hizo si za msingi, kwani kila mtu anao uhuru wa kuchagua kile akitakacho pasi na kulazimishwa, hivyo ni kilichofanyika ni kinyume cha haki za binadamu, kwa sababu baadhi ya watu walilazimishwa kumuunga mkono mgombea huyo ambaye ushindi wake unatiliwa shaka.
Tanzania Daima ilipowasiliana na Katibu wa CCM, Wilaya ya Lindi Mjini, Zainabu Chinowa, juu ya hatua hiyo ya kuwasimamisha kazi watendaji hao, hakuwa tayari kulitolea ufafanuzi huku akielekeza atafutwe mwenyekiti wa chama hicho wilaya, Said Manyanya.
Naye Mwenyekiti huyo wa CCM, Wilaya ya Lindi mjini, Said Manyanya, alisema yeye hana taarifa za kusimamishwa kwa watendaji hao huku akiahidi kuzifanyia uchunguzi taarifa hizo ili kubaini ukweli wake.
Katibu wa CCM Mkoa wa Lindi, Albert Mgumba, alipotafutwa kwenye simu yake ya mkononi ili kupata kauli yake, zimegongwa mwamba kutokana na kuzimwa.
Friday, October 29, 2010
Watendaji 50 wa CCM watimuliwa
Posted by Mafia Kisiwani at 5:08 PM
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment