Sunday, August 22, 2010

Mapingamizi yashamiri majimboni

na Mwandishi wetu




MAPINGAMIZI ya kupinga wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge yameendelea kuwasilishwa katika majimbo mbalimbali hapa nchini, huku idadi kubwa yakitupwa na wasimamizi wa uchaguzi.

Singida

Mgombea wa kiti cha ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Singida Mjini, Mohamed Dewji, amemuwekea pingamizi mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Isango Josephat, kwa madai ya kuwa na shaka na fomu zake za udhamini.

Dewji alisema kuwa fomu za Isango zinaonyesha hazikukaguliwa sehemu ya wadhamini na msimamizi wa uchaguzi, jambo ambalo anazitilia shaka kadi na saini za wanachama waliomdhamini.

Aliongeza kuwa pamoja na dosari hizo, mgombea huyo pia hakupendekezwa na chama chake siku alipochukua fomu Agosti 16 mwaka huu kama maelekezo ya tume ya uchaguzi yanavyoelekeza.

Dewji alisema fomu za Isango katika fomu yake ya uteuzi imethibitishwa na Yahaya Ramadhani, ambaye hana dhamana iliyoelekezwa na tume ya uchaguzi, kwani Yahaya Ramadhani ni katibu mwenezi wa CHADEMA wa wilaya na wala si katibu wa wilaya au mkoa kama ilivyoelekezwa kwenye fomu namba 8B kifungu C.

Dewji aliongeza kuwa kutokana na mgogoro uliojitokeza kwa Isango kuchukua fomu isivyo halali, fomu yake ya uteuzi haikusainiwa na uongozi wa kitaifa wa chama chake kama ilivyoelekezwa kwenye sura ya tano, kifungu cha 5.5, aya ya (iii) ya maelezo kwa vyama vya siasa na wagombea.

Mbeya

Wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo ya Mbeya Mjini na Vijijini, wametupilia mbali pingamizi mbili za wagombea ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), waliokatiwa kutokana na kukosa sifa.

Akizungumza na waandishi wa habari, msimamizi wa uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini, Juliana Malange, alisema walipokea pingamizi mbili zilizotolewa na mgombea wa CCM, Mchungaji Luckson Mwanjale dhidi ya wagombea wa CHADEMA na UDP, Sambwee Shitambala na Mboma Mwasyandele.

Malange alitaja baadhi ya sababu za kuwekewa pingamizi wagombea hao kuwa ni pamoja na mgombea wa CHADEMA kushindwa kuonyesha tarehe ya tamko, mtaa au kijiji katika kuainisha anuani ya makazi yake.

Aliongeza kuwa katika pingamizi la mgombea wa UDP, mtoa pingamizi alidai kuwa alikosea kuandika kwa usahihi jimbo aliloanisha kugombea kwa kuandika kuwa anagombea jimbo katika Halmashauri ya Mbeya Vijijini badala ya Mbeya.

Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dk. Samuel Lazaro, alitupa pingamizi mbili zizotolewa kwa madai ya kukosa vigezo.

Alisema pingamizi hizo zilitolewa na mgombea wa NCCR- Mageuzi, Agabo Mwamtobe, dhidi ya wagombea wa CCM na CHADEMA, Benson Mpesya na Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu.

Alisema katika pingamizi la mgombea wa CHADEMA, mweka pingamizi alitaka mgombea wa chama hicho athibitishe uhalali wa malipo ya tamko la kiapo.

Aidha, Dk. Lazaro alisema pingamizi kwa mgombea wa CCM lilikuwa likidai kuwa fomu ya mgombea huyo ilikosewa kujazwa tarehe ya uteuzi.

No comments: