Bakari Kimwanga
SALAAM aleikum, ndugu Waislamu mlio katika swaumu ikiwa leo ni Ramadhani ya kumi na moja tukiwa tayari tumengia kumi la pili ambalo kila mja anatakiwa kuzidisha swala za kumwomba msamaha Allah (S.W), aliyetupa uwezo wa kulianza kumi la pili kwa nguvu na wengi wetu tukiwa na imani ya kukubaliwa swaumu zetu kwa dhati mbele yake
Kumi la mwanzo la mwezi wa Ramadhani linajulikana ni kumi la rehema, ambapo waja hupewa rehema na Mwenyezi Mungu kwa kufanyiwa wepesi wa mambo yao ambayo wanakuwa wanayaomba hasa kwa wale ambao funga zao zilipokelewa na Mwenyezi Mungu.
Mwislamu atakapokuwa mgonjwa katika mwezi wa Ramadhani, anaumwa maradhi ambayo kupona kwake kutachukua muda mrefu au mzee mkongwe asiyeweza kufunga. Katika hali na mazingira haya, sheria inawaruhusu kutofunga lakini kwa wale walio na uwezo wanatakiwa kutoa kwa maskini nusu ya chakula kwa ajili ya futari kwa kila siku.
Kumi la pili limeanza ambalo ni la kuomba toba (msamaha), ni kumi la kuzidisha maombi na kuzidisha ibada kwani tuna nafasi muhimu tunayohitaji kuichunga kwa manufaa yetu ya ahera hapo baadaye, kumi ambalo kila mja mwenye yakini anahitaji kujiweka sawa ili awe mmoja wapo wa watakaosamehewa.
Waumini wa dini ya Kiislamu wakati huu ni wa thamani kubwa sana huzingatia kuwa hata kwa wanadamu kupeana misamaha baada ya makosa makubwa mazito tena yanayoonekana kwa macho yetu na hudhani tunaweza kuyasawazisha lakini yapo yale tunayojificha nayo.
Mwenyezi Mungu mwenyewe anayajua yote yaliyodhahiri na yaliyofichika na hata yaliyo ndani ya nia ya mwanadamu, basi ana sifa ya wema mkubwa pale anapotuambia niombeni nitakupeni na pale anaposema katika kitabu chake kitukufu cha Kurani “kuwa hakika hufuta makosa yote ya waja wake” ndiyo maana tulisema ni nafasi adimu ndani ya mwezi ambao amewaahidi waja wake msamaha tujiangalie wanadamu jinsi tulivyomkosea mengi muumba wa mbingu na ardhi, tupo tunaomshirikisha, tupo tunaodhulumiana roho na mali, tupo tuliosahau kwa kuwa na kipato, tupo tuliosubiria umaskini wetu vibaya, tupo tuliowaasi wazazi ndugu na jamaa.
Makosa kama haya yanahitaji kusafishwa na si kwa kitu kingine isipokuwa kutubia (kuomba msamaha kwa mola wetu), kwani Mwenyezi Mungu hutazama yalio nyoyoni na yadhahiri na humpima mja kwa kujitambua na kujutia makosa yake kwa kufanya toba ya kweli huku akimlilia msamaha Muumba wake (S.W). kwani Kurani inatuambia kuwa Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe.
Kinga kwa Mungu hutafutwa kwa maombi na matendo mema, wengi tumevuka mipaka ya mtu na kushindwa kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu, tufikirie yule mtu ambaye anatafuta mwanadamu mwenziwe amnyoshee mambo yake tena kwa dhamira ya kuharibu yaliyo mema au haki ya mwingine, ziko sifa ambazo zitolewazo kwa baadhi ya watu kwamba wanaona mbali na wengine huenda kutazamiwa kwa waganga wapiga ramli, hali inayosababisha kuwepo kwa uhasama.
Kurani inazuia Mwislamu iwe siku ya Ramadhani au nyingine kutokwenda kwa waganga wanaopiga ramli, kwani kwa kufanya hivyo utakuwa umeshiriki kumshirikisha huku ukimpatia sifa yule mganga kwa kumuona anaona yaliyojificha, hivyo sifa hiyo ya Mungu unaichukua kwake na kumpa mtu.
Kutokana na hilo, utakuwa umemshirikisha Mwenyezi Mungu uliyekwenda kwa mganga na mganga mwenyewe aliyejihusisha na kufanya hayo atakuwa ameukana Usilamu na Mwenyezi Mungu.
Katika kutaka msamaha wa Mwenyezi Mungu ni muhimu kwa mja kutambua aliumbwa kwa ajili gani na kuletwa hapa duniani kwa makusudi yapi na hata tukisoma katika Kurani tukufu tunaona wazi ‘Mwenyezi Mungu ameumba majini na watu ili wamuabudu yeye’.
Hata tukiangalia ngazi ya familia kuna baadhi ya wanawake huwa vipindi vyote hawataki kuwaheshimu waume zao lakini kwa yule mwenye kujitambua, ni katika kumi hili la pili anatakiwa kujutia makosa yake na kumtaka msamaha Muumba wetu wa mbingu na ardhi kwa kuzidisha ibada na toba ya kweli.
Allah (S.W) anasema: “Enyi mlioamini! Mmelazimishwa kufunga kama walivyolazimishwa waliokuwako kabla yenu ili mpate kumcha Mungu siku chache tu , na atakayekuwa mgonjwa katika nyinyi au katika safari (akafungua baadhi ya siku), basi atimize hesabu katika siku nyingine na wala wasioweza, watoe fidia kwa kumlisha maskini na atakayefanya wema kwa radhi ya nafsi yake, basi ni bora kwake, kufunga ni bora kwenu ikiwa mnajua ni mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa Kurani ili iwe uongozi kwenu na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi (wa baina ya yaliyo mema na yasiyo mema).
Atakayekuwa katika mji katika huu mwezi (wa Ramadhani) afunge na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hesabu katika siku nyingine. Allah, anakutakieni yaliyo mepesi na wala hakutakieni yaliyo mazito, na pia mtimize hesabu hiyo na kumtukuza Allah kwa kuwa amekuongozeni, ili mpate kushukuru.” Aya 2:183-185
Aya hii tukufu imeanza kwa kuwaita Waislamu kwa jina la imani ili kuiamsha imani ndani ya nyoyo zao na kuwaandaa kiroho kuitika na kupokea amri au maagizo watakayopewa kwa mujibu wa imani yao kwa sababu shani na tabia ya muumini wa kweli ni kumtii Mola wake mtukufu katika kila analomuamrisha kutenda au kutotenda, aya hii imebainisha ubainifu kamili na timilifu wa fadhila (ubora) ya swaumu ya Ramadhani, falsafa au hekima yake na rehema ya Allah mtukufu kwa waja wake kupitia fadhila hii ya swaumu.
Kwa nini tufanye hivyo, hali ambayo itasababisha swaumu kuwa za mitihani kwa baba kutokemea hali hiyo itakayosababisha kukosa radhi za Mwenyezi Mungu (S.W), ni muhimu kutoa maelekezo mema kwani hata ukiomba mkimlilia msamaha wa kweli, basi naye ataupokea kwa dhati kwani atakuwa ameshuhudia jinsi ulivyoiongoa familia katika jambo la heri.
Yarabi tukubalie toba zetu na utusamehe makosa yetu na zipokee funga zetu na sala zetu. Amen.
Sunday, August 22, 2010
Kumi la pili la Ramadhani lenye kuomba misamaha na kukubaliwa
Posted by Mafia Kisiwani at 12:05 PM
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment