Wednesday, April 7, 2010

Mpendazoe moto mkali CCM

• Awagawa wanachama na viongozi


na Ali Lityawi, Shinyanga




ZIKIWA zimebaki siku tatu kabla ya kuanza kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), hofu ya wabunge wengine kujiengua chama hicho na kujiunga na Chama cha Jamii (CCJ), imezidi kuongezeka, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Hofu hiyo inakuja wiki moja tangu mmoja wa wabunge machachari wa CCM, Fred Mpendazoe (Kishapu), kutangaza kujiengua ndani ya CCM na kujiunga na CCJ ambacho hadi sasa hakijapata usajili wa kudumu.

Habari ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka ndani ya CCM, zinadai kuwa baadhi ya wabunge wanaweza kutangaza kuhama CCM kutokana na shinikizo la makundi hasimu ndani ya Bunge na NEC, wanayotarajiwa kukamiana kwenye kikao hicho kilichopangwa kufanyika Aprili nane na tisa, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa habari hizo, shinikizo hilo ambalo linatarajiwa kuwapo kwenye ajenda ya mengineyo, litatolewa na kambi ya wabunge na wajumbe wa NEC waliojitosa hadharani kuwatetea makada na viongozi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Ajenda nyingine katika kikao hicho ni pamoja na suala la mgombea binafsi, gharama za uchaguzi, kujaza nafasi za Katibu Mwenezi CCM mkoa wa Dar es Salaam iliyoachwa wazi na Haji Manara na mkakati wa ushindi.

Wajumbe waliozungumza na Tanzania Daima Jumatano kwa sharti la kutotajwa majina yao, walisema kambi ya waathirika wa ufisadi na watetezi wao imepata nguvu, na sasa imeamua kuwaingiza wapiganaji wa ufisadi kwenye kundi la watu wanaotaka kujiunga na CCJ.

Hofu ya wabunge wapambanaji na makada wengine wa CCM imeongezeka baada ya taarifa za kuporwa kwa mkoba wa mwenyekiti wa CCJ Richard Kiyabo na watu wanaodaiwa kuwa wa idara usalama. Kunadaiwa kuwapo majina ya siri.

Baadhi ya wabunge waliokuwa wanajipambanua kama wapambanaji dhidi ya vita ya ufisadi mbali ya Mpendazoe ni pamoja na Spika wa Bunge, Samuel Sitta, Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela), Aloyce Kimaro (Vunjo), James Lembeli (Kahama), Anna Kilango (Same Mashariki), Lucas Selelii (Nzega), Christopher ole Sendeka (Simanjiro) na Beatrice Shelukindo (Kilindi).

Katika hatua nyingine, siku moja baada ya kufanyika kwa maandamano yaliyoitishwa na uongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga kwa lengo la kumshutumu Mpendazoe kujiunga na Chama cha Jamii (CCJ), chama tawala kimegawanyika.

Mmoja wa makada wa CCM waliopinga hatua hiyo ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Charles Gishuri, ambaye aliliambia Tanzania Daima Jumatano kuwa ni makosa kwa viongozi wa CCM kumfanyia maandamano, kumkashifu na hata kumsema kwamba alikuwa mzigo wa gunia la misumari.

Gishuri ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Mazingira ulioko mjini Shinyanga ambapo alitangaza nia yake ya kuwania ubunge katika Jimbo la Shinyanga kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi.

DC huyo ambaye katika mabadiliko madogo yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete juzi amehamishiwa katika wilaya ya Mbeya, alisema anawashangaa wana CCM walioandamana kwa lengo la kumtuhumu na kumshambulia Mpendazoe kwamba alikuwa mzigo kwao.

Alisema CCM mkoani Shinyanga ilikuwa na uwezo wa kumuita na kumuonya Mpendazoe katika vikao vya ndani baada ya kubaini upungufu na matatizo yake, lakini ilikaa kimya na sasa inamtoa kasoro baada ya yeye kuhama, jambo ambalo si sahihi.

“Mimi nashangaa kwamba wapo baadhi ya viongozi wa juu wa CCM waliomwita Mpendazoe alikuwa gunia la misumari walilokuwa wakilibebea kwa kipindi chote cha miaka minne na kusema kujiuzulu kwake hakutaiyumbisha CCM kwani chama hicho kina wanachama wengi, kauli hiyo si sahihi kabisa, tulipaswa tumsaidie, lakini si kumtolea maneno ya kashfa,” alisema DC huyo.

Alisisitiza kuwa maamdamano hayo yangekuwa na maana kama yangefanywa kwa lengo la kuwalaani baadhi ya viongozi wa juu wa CCM mkoani Shinyanga, akiwemo Mwenyekiti, Hamis Mgeja, na kumtaka ajiuzulu kwa kushindwa kumwongoza Mpendazoe hadi kufikia hatua ya kuwatelekeza wapiga kura wake.

Akijibu tuhuma hizo, Mgeja alisema kuwa CCM inamheshimu sana mwenyekiti huyo mstaafu na mkuu wa wilaya ya Njombe, hivyo haoni sababu ya kulumbana naye kwa sababu ya Mpendazoe.

“Mimi namshauri ndugu yangu, atangaze nia yake ya kuwania ubunge na aendelee kufanya kazi aliyokabidhiwa na rais ya kuwahudumia wananchi wilayani kwake, lakini asianze malumbano haya,” alisema Mgeja.

Mgeja alisema Mpendazoe hajawahi kuikosea adabu CCM, hivyo hawakuwa na sababu ya kumuita kwenye vikao vya maadili na aliyokuwa akizungumza bungeni kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya Kiwira, Richmond na mengineyo, yalikuwa ni haki yake kama mbunge na Katiba hairuhusu kumhoji mtu aliyetoa hoja ndani ya Bunge.

Hivi karibuni, Mpendazoe alitangaza kuihama CCM na kujiunga na CCJ huku akikishambulia chama chake cha zamani pamoja na mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais Jakaya Kikwete.

No comments: