Monday, March 29, 2010

CCJ yasaka wanachama kwa mtandao

na Shehe Semtawa



CHAMA cha Jamii (CCJ), kimezindua huduma ya kujiunga na chama hicho kwa kutumia ya ujumbe mfupi wa maandishi (sms).

Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Richard Kiyabo, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa chama hicho kimeamua kuzindua huduma hiyo ili kutekeleza kwa vitendo suala la sayansi na teknolojia kwa lengo la kuwafikia Watanzania popote walipo.

Alisema utaratibu huo mpya unakuwa historia nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla kwa kupata wanachama kwa njia ya elektroniki au teknolojia ya habari na mawasiliano (teknohama).

“Hatua hii imefanikiwa kutokana na uzoefu wa nchi nyingine na mafanikio yanayopatikana kutokana na mfumo huo,” alisema Kiyabo.

Aidha, aliwaomba Watanzania wote wapenda maendeleo na ustawi wa nchi kujiunga na chama hicho kwa wingi kwa kutumia utaratibu huo usiohitaji muombaji kutokwa na jasho na kusumbuka.

Mwenyekiti huyo aliahidi kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu mafanikio ya utaratibu huo.

Alisema chama hicho hakina wivu wala hulka ya ushindani wa kitoto, hivyo inavihimiza vyama vingine kujiunga na mpango huo wa teknolojia kwa faida ya taifa letu kwa kutoa msaada wa kitaalam kwa chama chochote kinachohitaji utaalamu huo.

Alisema katika muda wa wiki tatu tangu kilipopata usajili wa muda kimefanikiwa kupata wanachama 7,500 nchini.

Naye Katibu Mwenezi wa Chama hicho, Dickson Ng’hily, alisema utaratibu huo ni rahisi kwa kila mwanachama anayetaka kujiunga na CCJ, popote pale alipo ikiwa ni shamba, nyumbani, safarini au sokoni.

Alisema mwanachama anachotakiwa kufanya ni kutuma ujumbe mfupi wenye maandishi yenye neno CCJ kwenda namba 15337 na baada ya muda mfupi utakuja ujumbe utakaomtaka mwanachama kuandika neno sajili*jina kamili*tawi alipo*jimbo*mkoa na kutuma kwenda namba hiyo.

“Mwanachama akishafanya hivyo baada ya wiki tatu atapata kadi yake hapo hapo alipo,” alisema katibu mwenezi huyo bila kufafanua.

No comments: