Thursday, February 25, 2010

Waziri Wasira kortini

• Adaiwa sh mil 90/-

na Andrew Chale




WAZIRI wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam akidaiwa sh milioni 90 kwa kumdhalilisha na kumsumbua Mkurugenzi wa Kampuni ya Cargo Building, Andrew Ngai.

Kesi hiyo ya madai namba 24/2008 ilisikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Shamshana.

Alipotakiwa kujitetea, Wasira alishangazwa na uwepo wa kesi hiyo kwa maelezo kwamba yeye ndio mwenye haki ya kumdai mkurugenzi huyo hasara ya vigae 600 alivyopoteza.

“Nashangaa kusikia mimi nashitakiwa wakati mimi ndio nimepata hasara ya vigae vyangu 600 vilivyokuwa kwenye kampuni ya huyu bwana,” alieleza Wasira.

Kwa upande wake, Wakili Gasper Nyika anayemtetea waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa Bunda kupitia CCM, alidai maelezo ya awali yaliyotolewa na mteja wake mwaka 1999 yalionyesha kwamba aliagiza vigae 2,000 kutoka nchini Afrika Kusini na kumkabidhi Ngai anayeelezwa kuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Cargo Building.

Akiendelea kutoa maelezo yake, wakili Nyika alisema mteja wake alitumia vigae 1,400 na kubakiza 600 vilivyoelezwa kupotea kabla ya Wasira kufungua kesi ya madai dhidi ya Ngai, akitaka kulipwa sh milioni sita kama gharama za vigae 600 vilivyopotea. Hata hivyo, alishindwa kesi.

Baada ya kumbwaga Wasira mahakamani, Ngai alifungua kesi akitaka kulipwa sh milioni 90 kama fidia ya usumbufu na kudhalilishwa kwa kampuni yake.

Mahojiano kati ya waziri huyo na wakili wa mdai aliyejitambulisha kwa jina la Chabruma yalikuwa kama ifuatavyo:

Wakili: Kampuni uliyoikabidhi vigae inaitwaje?

Wasira: Iliitwa Cargo… nadhani imeshakufa hiyo kampuni yenyewe.

Wakili: Sasa ilikuwaje ukaishitaki kampuni ambayo haipo na hauijui?

Wasira: Kwa sababu mwenye kampuni ile tunaishi jirani.

Wakili: Unajua kwa nini Ngai alishinda kesi?

Wasira: Ni maamuzi ya mahakama… nami nilisikia kufutwa kwa kesi hiyo katika vyombo vya habari. Sasa mimi nashangaa kufunguliwa kesi kama hii.

Baada ya majibu kutoka kwa waziri huyo, wakili wa mdai aliomba kuahirishwa kwa kesi hiyo hadi Machi 12 ili wakajipange vema.

Hata hivyo ombi hilo lilikataliwa na mahakama na badala yake utetezi wa kesi hiyo utaendelea Aprili 12.

No comments: