Wednesday, February 24, 2010

Hatima ya CCJ kesho

• Viongozi wake wampa mtihani mzito Tendwa

na Irene Mark




HATIMA ya usajili wa muda wa Chama Cha Jamii (CCJ), ambacho Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, amekuwa akikipiga chenga, inatarajiwa kujulikana kesho katika mkutano kati yake na viongozi wa chama hicho.

CCJ, chama ambacho kimesababisha mtikisiko ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimekuwa kikipigwa kalenda na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa karibu miezi miwili sasa tangu kuwasilisha maombi yao ya usajili wa muda Januari 20, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya msajili, Tendwa ambaye amekuwa safarini Arusha na kuingia ofisini jana, amepanga kukutana na viongozi wa CCJ kesho ofisini kwake.

Wakati Tendwa akiwa kwenye mtihani mzito wa kukipa usajili wa muda chama hicho, viongozi wa CCJ; Katibu Mkuu Renatus Muabhi na Mwenyekiti wake, Richard Kayabo, kwa nyakati tofauti, waliliambia Tanzania Daima Jumatano jana kwamba wamekamilisha taratibu zote za usajili.

“Sisi tunamsubiri msajili, sijui atatupa visingizio gani tena, hatuna kitu kingine tunachodaiwa maana kila kitu anajua yeye... tutamsikiliza, lakini tunachohitaji sasa ni usajili wa chama chetu, tumeshakaa vya kutosha,” alisema Kayabo.

Hata hivyo habari zaidi ambazo Tanzania Daima Jumatano imezipata, zinadai kuwa CCJ kimekamilisha mambo mengi ya msingi ikiwa ni pamoja na kuweka sahihi za wanasheria katika baadhi ya nyaraka pamoja na kukabidhi bendera ya chama hicho katika ofisi ya msajili.

Habari zaidi zinasema kuwa hatua iliyofikiwa sasa na CCJ inamuweka katika wakati mgumu Tendwa kukisajili chama hicho kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni vitisho kutoka kwa baadhi ya viongozi wa CCM wanaotaka kisipewe usajili.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, kadi za CCJ zimekaa muundo sawa na kadi ndogo ya kuchukulia fedha kwenye mashine maalumu za benki maarufu kama ATM huku kwa nyuma zikiwa na picha ya Mwalimu Nyerere, tofauti na nyingine ambazo ni kubwa kama za CCM.

Duru za kisiasa zinauangalia ujio wa CCJ kama tishio kwa CCM na Rais Jakaya Kikwete, kutokana na kutajwa kuhusisha vigogo wa chama hicho tawala ambao wanataka kujitenga na kugombea urais Oktoba mwaka huu.

Tayari Spika wa Bunge Samuel Sitta, aliwahi kusema kwamba haoni tatizo la kusajiliwa CCJ, huku pia akisema hawezi kuzuia watu kumuhusisha na chama hicho kama mgombea hapo Oktoba.

CCJ imekuwa ikitikisa nchi tangu taarifa zake kuchapishwa kwenye vyombo vya habari, kwani kuna majina makubwa yanatajwa kuwemo akiwemo Spika Sitta, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba, John Malecela. Lakini wote wamekanusha.

No comments: