Friday, July 15, 2011

Serikali imechukua hatua kuhusu ripoti za CAG?

Elias Msuya
KWA muda mrefu sasa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa fedha za serikali (CAG) amekuwa akieleza jinsi idara mbalimbali za serikali zinavyotumia vibaya fedha za walipa kodi.Lakini taarifa hizo, serikali inaziona kama porojo tu. Kwanini? Kwa sababu hakuna hatua zozote zinazochukuliwa na serikali dhidi ya watendaji wake wanaohusika.

Kwa mfano taarifa iliyotolewa na CAG kwa wajumbe wa mkutano cha chama cha Serikali za Mitaa – ALAT, walipokutana Dar es Salaam hivi karibuni inaonesha kuwepo kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha na rasilimali katika halmashauri nyingi nchini.Alitaja halmashauri tano zinazoonekana vinara kuwa ni pamoja na Rombo, Kilosa, Rorya, Tarime na Manispaa ya Sumbawanga.

Alitoa mfano wa posho za safari walizolipana watendaji kwa halmashauri za Rombo na Kilosa, akisema kulikuwa na Sh 203,379,000 zilizolipwa isivyo halali huku madaftari ya mahudhurio yakionesha kuwa watumishi hao walikuwepo kazini kwenye vituo vyao.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo mafuta ya magari yenye thamani ya Sh 64,581,030 yanaonekana kutumika bila kuwa na maelezo sahihi.Kwa upande wa elimu taarifa hiyo inaonesha kuwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo walitumia vibaya fedha za elimu kiasi cha Sh 31,020,000, ikijumuisha tuhuma za wizi wa wino wa mashine ya chapa wenye thamani ya Sh.14,635,000 na wino wa mashine ya kutolea nakala wenye thamani ya Sh 16,385,000.

Vilevile imeonyesha kukosekana kwa hati za malipo zenye thamani ya sh 766,489,920 wakati wa ukaguzi katika Halmashauri ya wilaya ya Kilosa.Kama hiyo haitoshi CAG ametaja matukio sita ya wizi wa fedha katika halmashauri ya Wilaya ya Kilosa yanayohusiana na ubadhirifu wa fedha wa kiasi cha Sh 277,026,849 uliosababishwa na udhaifu katika udhibiti wa mfumo wa ndani wa halmashauri ambapo, usuluhisho wa benki ulifanywa na watumishi wasio waaminifu, pia haukutengenezwa kwa wakati.

Kulikuwa pia na malipo ya awali kwa wakandarasi kinyume na kiwango kinachokubalika ambapo baadhi ya wakandarasi wilayani Kilosa walikuwa wakipewa malipo ya awali kwa kiwango cha asilimia 30 hadi 70 ya fedha ya mkataba kinyume na kiwango cha asilimia 15 kilichoidhinishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma( PPRA).

Wilaya hiyo pia imepata hasara katika ukusanyaji wa mapato ambapo imetumia jumla ya Sh 119,614,000 ili kukusanya kiasi cha Sh.57,226,690 hivyo kusababisha hasara ya Sh.62,387,110.Mbali na kupata hasara kwenye wilaya hizo kumekuwa pia na tatizo la kutoingiza mapato kwenye vitabu vya fedha. Kwa mfano kiasi cha Sh 7,380,000 kilichopatikana kutokana na mauzo ya viwanja katika mji wa Holili uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo hazikuingizwa katika vitabu vya fedha vya Halmashauri.

Kiasi hiki kinajumuisha Sh2,785,000 ambazo zilitokana na wizi wa kutumia kalamu na Sh4,595,000 zilizowekwa kwenye akaunti ya mtu binafsi.Hizo ni baadhi tu ya takwimu zilizotajwa na CAG hasa kwa kuwa ndiyo zimeshikilia rekodi ya ubadhirifu. Lakini upo ubadhirifu mwingine mwingi tu unaoendelea katika halmahsauri za wilaya na manispaa nchini.

Licha ya kuwepo kwa ofisi ya mkaguzi na mdhibiti wa fedha za serikali anayejitahidi kufichua uozo huo, serikali imekaa kimya.Wakati fedha hizo zikifujwa, hali ya maisha ya wananchi huko vijijini ambao ndiwo walipa kodi hizo zinazofujwa inakatisha tamaa. Wanafunzi hawana madarasa, madawati wala vifaa vya kufundishia. Walimu wanadai malimbikizo ya fedha zao.

Huduma ya maji ni kitendawili kisicho na mteguaji, umeme ndiyo haupo kabisa, barabara hazitamaniki wakati wa mvua. Siyo kwamba fedha hazipo, hapana. Tatizo kuna mchwa kwenye halmashauri hizo ambao kazi yao ni moja tu, kutafuna fedha za umma.

Baadhi ya wakurugenzi kwenye mkutano huo walilalamika kuhamishiwa watendaji walioshindikana kwa wizi na ubadhirifu. Wakibainika kuwa na makosa wanakwenda wizarani na kuomba uhamisho, wanahamia halmashauri nyingine na kuendelea kutafuna kama kawaida. Hayo nayo Waziri wa Tamisemi hayajui?

Siyo kwamba watendaji hao hawajulikani. Hata wakati CAG akitoa taarifa yake waliohusika walikuwa wakimsikiliza na mwisho wa yote wamekomba marupurupu ya semina na kuondoka.

Mawaziri nao walikuwepo kwenye mkutano huo. Waziri mkuu Mizengo Pinda ndiye aliyefungua mkutano huo. Walikuwepo pia Waziri wa Sheria na Katiba Celina Kombani, Naibu Waziri wa Tamisemi Aggrey Mwanri na Waziri wa nchi katika ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu Steven Wassira.Wamesikiliza uozo huo na wamekuwa wakiusikia mara kwa mara, lakini hakuna hatua yoyote inayochukuliwa.

Nilitegemea kusikia katika mkutano huo, walau wajumbe wakatoka na azimio la kuwawajibisha wafujaji wa fedha za umma ili kujenga upya msingi wa maendeleo, lakini hakuna lolote.

Hii inaonyesha kuwa serikali yetu imejaa viongozi wa maneno, wasiojua kuchukua hatua hata kwenye makosa ya wazi.Nadhani hii sasa inatosha. Kama viongozi waliingia madarakani kuwatumikia Watanzania hebu wachukue hatua ili kunusuru maisha ya Watanzania yaliyozama kwenye ufisadi.

Elias Msuya ni mwandishi wa makala wa gazeti la mnwananchi; 0754 897 287

No comments: