Sunday, July 24, 2011

Mandojo na Domokaya Baada ya kimya kingi, waibukia Fiesta 2011


Herieth Makwetta,
WASANII wakongwe wa muziki wa kizazi kipya, Joseph Francis Michael 'Mandojo' na Precioust Juma 'Domokaya', walikuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa burudani ya muziki mjini Moshi na Arusha kwenye tamasha la Serengeti Fiesta wiki iliyopita.

Pamoja na kuwepo kwa idadi kubwa ya wasanii waliopanda jukwaani kwenye tamasha hilo, Wawili hao ambao waliwahi kutamba na kibao cha Wanokonoko mwanzoni mwa miaka ya 2000 walichomshirikisha Lady Jay Dee, walitumbuiza jukwaani kwa muda wa dakika 45 pasipo kuwachosha mashabiki.

Hii ni nadra sana hasa kwa wasanii wetu wa hapa nchini kwani wengi wao wamekuwa ni wavivu pindi wawapo jukwaani na wengine wamediriki kuimba bila hisia wala hamasa kwa mashabiki wanaowapenda.

Inaweza ikawa ni dalili kwamba muziki wa kizazi kipya unapoteza mwelekeo, kwani umahiri wa wasanii wakongwe unajionyesha hadharani na kupendwa zaidi na mashabiki ukitofautisha na ule wa chipukizi.

Katika mahojiano na wasanii hawa waliweza kunieleza mawili matatu ambayo huenda ni maswali ambayo msomaji ulikuwa ukijiuliza kwa muda mrefu.

Mwandishi: Imekuwa ni kama 'suprise' kuwaona hapa jukwaani ilikuwaje mbona ni kama mlipotea kwenye fani?

Domokaya: Ni muda mrefu sasa hatujawa kwenye fani, lakini si kwamba tumeacha muziki, bado tunafanya vema. Imekuwa kama kuwashtua mashabiki lakini si kwamba hatuwezi tena muziki ni wazi tumefanya vizuri na nadhani wengi wameona nini tumefanya.

Mwandishi: Lakini ni kweli kwamba bado mna nguvu za kupambana na wasanii chipukizi?

Mandojo: Ng'ombe hazeeki maini. Bado tuna nguvu na kuhitajika na mashabiki. Chipukizi wana nafasi yao lakini hata sisi pia tuna nafasi zetu. Inapopatikana nafasi kama hii lazima tuhakikishe tunafanya kile ambacho tumekubaliana kimkataba na si lelemama.

Domokaya: Unajua linapofikia suala kama hili, bila shaka hatuachi nafasi kubwa kati yetu na promota ambaye ametupa kazi. Hili ni tatizo ambalo wasanii wengi chipukizi wanalo, hawathamini ile nafasi wanayopewa na mapromota hawa wanaoandaa matamasha likiwemo hili la Fiesta, ni heshima kubwa. Hivyo lazima uhakikishe unawafanya mashabiki wako wakuone unafaa na kukonya nyoyo zao.

Mwandishi: Mnadhani muziki wa bongofleva kwa sasa umepoteza mwelekeo?

Domokaya: nadhani ni wakati mzuri kwa wapembuzi wa masuala ya burudani ya muziki kutambua kwamba wakongwe wana nafasi kubwa sana kuliko chipukizi kwa sasa, kwani bongo fleva ya zamani zi ile ya sasa kwani inadumu na haipotezi ladha.

Mandojo: Kwa upande wangu naona umepoteza mwelekeo, kwani sisi tuliimba mapenzi lakini yenye kufundisha na hata nyimbo zingine hazikuwa mapenzi lakini zilielimisha na kufundisha lakini kwa sasa mtu akiimba wimbo mapenzi yanazidi sana, licha ya hivyo bado hazikai zinachuja mapema.

Mwandishi: Mmesema kuwa mmerudi tena kwenye fani mmejipanga vipi.

Mandojo: Tuliwahi kuimba na Lady Jay Dee mwanzoni mwa miaka ya 2000 wimbo wa wanoknok, lakini hivi sasa tutarudi tena tukiwa na Jide na tunategemea kutoa kazi ambayo itakonga nyoyo za mashabiki.

Mwandishi: Bado mnaimba kwa vinanda kama zamani au?

Domokaya:Hapana kwa sasa tunafanya 'live band', kila siku ya Alhamisi tupo pale Nyumbani Loung kwa Jay Dee. Muda mwingi tumekuwa tukiandaa kazi zetu ambazo tunatarajia kuziachia mapema mwaka huu, kwa hiyo mashabiki wakae mkao wa kula.

Mandojo: Tumeandaa nyimbo kama 'Baba Kidawa' ambao tumetengeneza katika studio ya 'Marko Chali' tukiwa katika kundi la Wamandavaku ambalo tumewaingiza vijana wawili.

Mwandishi: Hii inamaanisha kwamba kwa sasa kundi la Mandojo na Domokaya halipo na badala yake kuna Wamandavaku?

Mandojo: Hapana, sisi tutabaki kuwa kama sisi na kundi ni baadaye.
Mwandishi: Je mna lolote la nyongeza?.
Man na Domo: Zaidi ni kuwajulisha washabiki wetu kuwa tumerudi upya waje washuhudie mambo yetu.
Mwandishi: Kazi njema
Man na Domo: Pamoja

No comments: