Friday, February 25, 2011

Simba, Yanga zawindana

na Dina Ismail




HOMA ya pambano la watani wa jadi katika soka hapa nchini, Simba na Yanga imeanza kupanda ambapo kamati za utendaji za timu hizo zikijipanga kukutana kwa ajili ya kuweka mikakati ya kuibuka na pointi tatu muhimu.

Wakati Yanga ikitarajiwa kukutana keshokutwa Jumapili, Simba inatarajiwa kukutana wakati wowote kuanzia sasa.

Vigogo hao wanatarajiwa kumenyana Machi 5, katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom itakayopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Timu hizo, zinaendelea kujifua kwa ajili ya mechi nyingine za ligi hiyo, ambako wachezaji wa Simba waliingia kambini juzi, huku Yanga wakifanya mazoezi ya kwenda na kurudi.

Ofisa habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema jana kwamba, kamati ya utendaji itakutana Jumapili kujadili masuala mbalimbali ya timu hiyo, hususani mwenendo wake katika ligi hiyo.

“Pamoja na hilo, pia watajadili mustakabali wa timu katika harakati za kuwania ubingwa,” alisema.

Sendeu alisema, wachezaji wote wako katika hali nzuri, huku kiungo wake aliyekuwa majeruhi Shamte Ally akianza mazoezi magumu na wenzake.

Kwa upande wa Simba, wachezaji wake wote wameingia kambini hoteli ya Lamada jijini Dar es Salaam, huku wachezaji wote waliokuwa majeruhi wakipona isipokuwa Uhuru Seleman.

Katika hatua nyingine, kituo cha televisheni cha Super Sports cha Afrika Kusini, jana kilirekodi mazoezi ya timu ya Yanga yaliyokuwa yakifanyika uwanja wa Kaunda.

Aidha, kituo hicho kilifanya mahojiano na kocha mkuu Sam Timbe, nahodha Shadrack Nsajigwa ‘Fusso’ na kipa Ivan Knezevic.

No comments: