Saturday, January 8, 2011

Wafanyakazi TANESCO waikalia koo serikali

na Bakari Kimwanga
WAFANYAKAZI wa shirika la umeme nchini (TANESCO) wameitaka serikali na viongozi wa kisiasa kuacha kuingiza maamuzi yao ya kisiasa ndani ya shirika hilo kwani yanakwamisha utendaji kazi.

Kauli hiyo waliitoa jana wakati wakizungumza katika mkutano baina ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, pamoja na wafanyakazi wa shirika hilo wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Wakitoa dukuduku lao, wafanyakazi hao walisema ili kuboresha miundombinu ya umeme nchini ni lazima serikali iepuke kuchukua maamuzi ya kisiasa kama ilivyotokea kwenye kampuni za IPTL na Songas.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi katika mkutano huo mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa TANESCO, Abdul Mkama, alisema ili kuondokana na tatizo la umeme ni lazima maamuzi ya kisiasa yaepukwe na kuliweka taifa katika hali ya usalama.

“Ni lazima tusema maamuzi ya kisiasa ndio yanayokwamisha utendaji kazi ya TANESCO, miaka mitatu iliyopita Waziri Mkuu mmoja alikwenda katika visima vya gesi vya Songas na kuwataka wananachi kuhama ili kupisha mradi wa umeme lakini imekuwa kinyume; ni lazima hili lizingatiwe kwa makini ili kuliokoa shirika hili,” alisema Mkama.

Aidha alisema kitendo cha serikali kutokuwa makini na mikataba hasa ya miradi ya umeme ya IPTL na Songas, kimesababisha kujengeka kwa chuki kati ya TANESCO na wananchi hali ambayo haitakiwi hasa katika zama hizi.

Katika hotuba yake Waziri Ngeleja, alisema ukweli miongoni mwa wafanyakazi ni lazima uheshimiwe kwani kila raia ana haki ya kulisaidia taifa ili kuondokana na dhana potofu iliyojengeka hasa kwa wananchi.

Alisema kwa kulizingatia hili serikali ya awamu ya nne kupitia Wizara ya Nishati na Madini ina mikakati ya muda mfupi na mrefu ili kuhakikisha suala la mgao wa umeme linakuwa ndoto ifikapo mwaka 2015.

Katika hilo pia alisema kuna changamoto ya kuwepo bei ya umeme zisikidhi gharama halisi za uendeshaji na usambazaji wa nishati hiyo.

Alisema ili kuhakikisha wanakabiliana na hali hiyo ni wajibu wa bodi ya TANESCO iboreshe huduma zake kwa wateja na kupunguza upotevu wa umeme na kuimarisha mifumo ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji.

Akijibu maswali ya wafanyakazi waliotaka kujua hatua ya serikalia juu ya hatima ya kiwanda cha magogo ya kiwira amabacho kinamilikiwa na TANESCO alisema ni jambo muhimu kukaa na kuzungumza kwa pamoja na kutoa mapendekezo yao kwa mujibu wa sheria.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO William Mhando, alisema shirika hilo liko mbioni kuanzisha kituo cha miito kwa wateja ambacho kitaanza mwishoni mwa mwezi Januari.

Alisema ni muhimu serikali kutoa msamaha wa kodi hasa ya kuagiza mafuta na vipuri vya mitambo ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuunganisha umeme kwa wateja wapya.

Mhando pia alisema ni muhimu wizara iendelee kushauri na kuelekeza ili kutekeleza kikamilifu majukumu na azma ya kutoa huduma bora ya umeme kwa manufaa ya Watanzania.

No comments: