Wednesday, January 5, 2011

Vigogo wagoma kutangaza mali zao

na Asha Bani
VIONGOZI wa siasa 3,047 nchini, wamegoma kurejesha fomu zinazoonyesha kiasi cha mali na fedha wanazomiliki kihalali.
Katika kundi hilo la viongozi wa siasa, wamo viongozi waandamizi wa serikali 470 ambao hadi Desemba 31 ambayo ni siku ya mwisho ya urejeshaji wa fomu hizo, walikuwa hawajawasilisha na hakuna maelezo yaliyotolewa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda, alisema kati ya viongozi wa siasa 4,346 waliotumiwa fomu za kuorodhesha mali zao 3,047 hawakurejesha na 1,446 tu, ndio waliorejesha.

Akitoa ufafanuzi wa viongozi wa siasa kwa makundi ya kikanda, Jaji Kaganda alisema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, viongozi 631 walitumiwa fomu hizo na kati yao 343, ndio waliorejesha, 288 waligoma kufanya hivyo.

Katika Kanda ya Magharibi, viongozi 540 waliotumiwa fomu, wawili kati yao ndio waliorejesha, 538 hawajarejesha wakati katika kanda ya kati, waliotumiwa fomu walikuwa 430, waliorejesha 145 na wasiorejesha ni 285.

Akizungumzia Kanda ya Kaskazini, alisema wanasiasa waliotumiwa fomu walikuwa 551, waliorejesha 127 na wasiorejesha 424 na katika Kanda ya Ziwa, wanasiasa 738 walitumiwa fomu, waliorejesha 251 na wasiorejesha ni 487.

Katika Kanda ya Kusini, waliotumiwa fomu ni 583, waliorejesha 312 na wasiorejesha 476, huku katika kanda ya makao makuu, walitumiwa fomu ni 875, waliorejesha 266 na wasiorejesha ni 609.

Jaji Kaganda alielezea tathmini ya urejeshaji ambapo alisema imeonyesha kuwa kumekuwa na ongezeko la viongozi wengi kutowajibika kutekeleza matakwa ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma ya mwaka 1995.

Hata hivyo alisema mwitikio kwa viongozi wa siasa unaweza kutafsiriwa kuwa ni mdogo kwa sababu kundi hilo linabebwa kwa kiasi kikubwa na madiwani ambao alidai taratibu za uteuzi na uundwaji wa mabaraza ya halmashauri nyingi mchakato wake ulikuwa bado haujakamilika.

Alisema hadi kufikia Desemba 31 mwaka jana, madiwani 1,032 kati ya 3,876, sawa na asilimia 26.62 ya madiwani wote, walirejesha fomu hizo za tamko.

"Hii inamaanisha kuwa jumla ya madiwani 2,844 sawa na asilimia 73.37 hawakuweza kurejesha fomu hizo, hivyo taratibu za kuwafikia zinaendelea kufanyika ili kila mhusika aweze kuwajibika kutekeleza sheria hiyo" alisema Jaji Kaganda.

Akizungumzia kuhusu watumishi wa umma alisema viongozi 4,064 walitumiwa fomu hizo, waliorejesha 2,324 wasiorejesha ni 1,741.

Akitoa ufafanuzi wa kikanda alisema katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini watumishi wa umma 272 walitumiwa fomu kati yao waliorejesha ni 167 na wasiorejesha ni 105, Kanda ya Magharibi waliotumiwa fomu 214, waliorejesha 74 na wasiorejesha ni 140.

Kanda ya Kati, watumishi waliotumiwa fomu walikuwa 273 walirejesha 100 na 173 hawakurejesha wakati katika Kanda ya Kaskazini waliotumiwa fomu ni 371, waliorejesha 228 na wasiorejesha 143.

Aliongeza kuwa katika Kanda ya Ziwa, waliotumiwa fomu ni 284 waliorejesha 183, wasiorejesha 101 na Kanda ya Kusini, waliotumiwa fomu 193, waliorejesha 106 na wasiorejesha 87.

Alifafanua kuwa katika ofisi ya Kanda ya Makao Mkuu, watumishi 2,457 walitumiwa fomu, waliorejesha 1466 na wasiorejesha ni 992.

Alisema hali ya urudishaji wa fomu kwa viongozi wa umma, imeathiriwa na kundi la Mahakimu ambao wanakadiriwa kufikia 1,631 sawa na asilimia 40.13 ambao wameshindwa kurejesha fomu kutokana na hali ya kijiografia na mawasiliano magumu nchini.

"Hii inamaanisha kuwa ukiondoa kada ya mahakimu, viongozi 109 wandamizi wa utumishi wa umma kati ya 2,433 ndio waliowasilisha fomu zao za tamko kwa wakati. Hii ni sawa na asilimia 4.48 ya kundi hilo" alisema Jaji Kaganda.

Kufuatia hali hiyo, alisema wahusika watapewa nafasi ya kujieleza ili wabainishe sababu za kutokutekeleza sheria hiyo.

Alisema hata hivyo hatua mbalimbali zitachukuliwa kwa viongozi hao ikiwa ni pamoja na kupewa nafasi ya kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua zaidi kwa mujibu wa sheria.

Alisema kama maelezo yao hayataridhisha, viongozi husika wataitwa mbele ya baraza la maadili ambalo litawasikiliza na kutoa mapendekezo kwa kamishna wa maadili juu ya hatua zinazofaa kuchukuliwa dhidi ya kiongozi hao.

"Taarifa ya Baraza itawasilishwa kwa Rais na nakala kwa Spika kwa hatua mbalimbali za kiutumishi na kiutawala sambamba na kusimamia kwa nguvu utekelezaji wa sheria kwa kuhakikisha kuwa mamlaka za nidhamu za viongozi husika zinawajibika ipasavyo kutekeleza mapendekezo ya sekretarieti dhidi ya viongozi wasiotekeleza misingi ya maadili" alisema Jaji Kaganda.

Akijibu swali kwa mwandishi aliyetaka kujua viongozi wangapi wameshaitwa na kuhojiwa kuhusiana na maadili mabovu wakiwemo wanasiasa na watumishi wa umma, alisema baraza limeanzishwa Julai mwaka jana hivyo halijakaa kuanza kujadili watu hao.

Alisema licha ya Baraza hilo kutoanza kazi, siku chache zijazo linatarajia kuwaita na kuwahoji kuhusiana na malalamiko mbalimbali yaliyotolewa dhidi yao.

Aidha alitoa ushauri kwa viongozi wa umma na wa kisiasa kufanya kazi kwa maadili kwa maslahi ya wananchi na sio ya mtu binafsi ili kujenga msingi ya utawala bora.

No comments: