Sunday, August 22, 2010

Laana ya Zitto balaa

• Yawanyonga wabunge kumi wa CCM


na Mwandishi wetu
MASIKITIKO na laana aliyoitoa Mbunge anayemaliza muda wake wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), kwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliochangia mbunge huyo kusimamishwa ubunge mwaka 2007, imewakumba na kuwaondoa madarakani wabunge zaidi ya kumi.

Wabunge hao ni wale walioipinga vikali hoja binafsi ya Zitto iliyolitaka Bunge liunde kamati teule ya kuchunguza utiaji saini wa mkataba wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi uliofanywa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi.

Aidha, wabunge hao mbali na kuipinga hoja ya Zitto, walishabikia hoja ya kutaka Zitto achukuliwe hatua kwa madai ya kusema uongo bungeni, iliyotolewa na mwenzao, Mudhihir Mudhihiri, ambaye ni mbunge wa Jimbo la Mchinga anayemaliza muda wake.

Wabunge hao ambao Zitto aliwalaani kuwa hawatarudi bungeni 2010, ni miongoni mwa wanasiasa walioangushwa katika kura za maoni za CCM na hivyo kukosa nafasi ya kutetea ubunge wao.

Waliokumbwa na laana hiyo ya Zitto ni Nazir Karamagi (Bukoba Vijijini), Siraju Kaboyonga (Tabora Mjini), Manju Msambya (Kigoma Kusini) na William Kusila (Bahi).

Wengine ni Ruth Msafiri (Muleba Kaskazini), John Malecela (Mtera), Mudhihir Mudhihir (Mchinga), Ponsiano Nyami (Nkasi) na Suleiman Kumchaya (Lulindi).

Akichangia hoja hiyo, Malecela alikwenda mbali zaidi kwa kumfananisha Zitto na mwiba kuwa wasipoutoa mapema utaleta madhara makubwa kwa serikali ya CCM ambayo itaonekana inasema uongo bungeni.

Hoja ya msingi ya Zitto ilikuwa ni kutaka Bunge liunde kamati teule ya kuchunguza utiaji saini wa mkataba huo uliofanywa mjini London nchini Uingereza kinyume cha taratibu, kwani Rais Kikwete alikuwa ameshatoa tamko kwamba serikali isingeingia mkataba mpya na mwekezaji mpaka na sheria ya madini iliyokuwepo ipitiwe na kuboreshwa.

Katika hoja yake hiyo, mbunge huyo pia alitaka kuondolewa kwa kipengele katika Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 1973 kuhusiana na asilimia 15% ya nyongeza kwenye mtaji wa uwekezaji ambao haujarejeshwa.

Hata hivyo, hoja hiyo haikupewa uzito kutokana na wabunge wa CCM kutumia wingi wao bungeni kuipinga na badala yake kuibua hoja mpya ya kutaka mbunge huyo aadhibiwe kwa kusema uongo bungeni na kumsingizia Karamagi.

Mudhihir alipoibua hoja hiyo alitumia kanuni ya Bunge ya 50 (1) inayozungumzia kumsemea mbunge mwingine uongo, kumpaka matope na kumdhalilisha.

Pia alitumia kanuni ya 59(3) alipoomba Bunge limpe adhabu ya kumsimamisha kazi ya ubunge Zitto ili iwe fundisho kwa wabunge wenye tabia ya kuwabambikizia wenzao makosa.

Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge hao na Zitto kusimamishwa kuhudhuria mkutano wa nane na wa tisa wa Bunge kabla ya kurejea bungeni baadaye baada ya adhabu hiyo.

Hata hivyo, wabunge hao baadaye walikuja kuonekana kuwa ni wasaliti kwa nchi kwa kudaiwa kuweka mbele zaidi masilahi na matakwa ya chama chao (CCM), kuliko masilahi ya taifa.

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, alionekana kutokubaliana na uamuzi huo wa makada wenzake, kwani aliamua kumteua Zitto kuwa mjumbe wa kamati maalum ya kupitia mikataba mibovu ya madini. Kamati hiyo ilikuwa chini ya Jaji mstaafu, Mark Bomani.

Uamuzi huo wa Kikwete ulitafsiriwa na wajuvi wa masuala ya kisiasa kuwa pigo kwa wabunge waliokuwa mstari wa mbele kumuadhibu Zitto kwa kuzungumzia mkataba tata uliosainiwa katika mazingira yaliyozua maswali mengi.

Baadhi ya wananchi, wanaharakati na wanasiasa waliopata kutoa maoni yao kwenye vyombo vya habari na mikutano ya hadhara waliweka wazi kuwa laana ya Zitto itawashukia wabunge hao na watapata wakati mgumu kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

Kabla ya Bunge kufikia hatua hiyo ya kumsimamisha ubunge Zitto, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alimpa nafasi ya kujieleza ambapo mbunge huyo alitoa nukuu ifuatayo:

“Mwaka 1978, pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kulikuwa na jarida linaitwa Cheche, serikali ikalifungia jarida hili. Katika toleo la mwisho la jarida hili la Cheche walisema hivi. ‘You can burn organisations, you can liquidate people, but revolutionary ideas never die.”

“Inaweza ikatolewa hoja, nimetimiza wajibu wangu, maamuzi ni ya Bunge, moyo wangu ni mweupe, ni jukumu la Bunge kuweza kuamua na kutoa uamuzi.

“Ninachoomba tu nitendewe haki, nipewe haki ya kusikilizwa kwa sababu haki ya kusikilizwa ni haki ya msingi kabisa, kwa hiyo kama kuna hoja yoyote ya kuniadhibu kwa vyovyote vile na bahati nzuri Mheshimiwa Spika ni mwanasheria; kwa vyovyote vile nitapata the right of hearing,” alisema Zitto.

Zitto aliongeza maneno haya: “Mheshimiwa Spika, I am a democrat. Niko tayari kwa maamuzi yoyote Bunge litakayochukua!”

Baada ya Bunge kumsimamisha, Zitto kwa kushirikiana na wapinzani wenzake, walizunguka baadhi ya mikoa kuelezea utata wa kusainiwa kwa mkataba huo pamoja na maamuzi ya kibabe ya Bunge.

Ziara hizo zilichangia kwa kiasi kikubwa kuzidisha umaarufu wa Zitto na wabunge wa kambi ya upinzani, ambao walionekana kujali zaidi masilahi ya wananchi kuliko wabunge wa chama tawala.

No comments: