Monday, March 29, 2010

Zitto, Ndesamburo wayateka majimbo

• Moto wa Zitto watikisa Jimbo la Geita

na Sitta Tumma na Charles NdagullaCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimezidi kuonyesha dalili za kuendelea kujiimarisha katika maeneo mbambali nchini, kadri siku za kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba zinavyozidi kujongea.

Baada ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, kuongoza harakati za kuuteka mkoa wa Dodoma, upepo unaonekana kuzidi kuvuma kwa chama hicho kuendelea kujizatiti katika maeneo mengine nchini.

Katika hatua ambayo haikutarajiwa, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, jana aliwasha moto wa aina yake wa kisiasa katika wilaya ya Geita alikopita na kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara wa wananchi waliojitokeza wakitaka ajitokeze kugombea ubunge katika jimbo hilo.

Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, alitumia fursa ya mkutano huo wa hadhara kutangaza hatua yake ya kuyaondoa majimbo mawili ya Kinondoni na Kahama katika orodha ya majimbo matano ambayo alikuwa ana nia ya kuchagua mojawapo na kugombea.

Akihutubia mkutano huo mkubwa, Zitto alisema kutokana na jinsi hali ilivyo bado alikuwa akiendelea kutafakari kuhusu uamuzi wa kugombea katika moja ya majimbo matatu ya Kigoma Kaskazini, Kigoma Mjini na Geita.

“Nawaombeni sana wana Geita mwaka huu tuichukue halmashauri ya hapa Geita kwa ubunge na udiwani katika maeneo yote…leo sitamki nitagombea wapi,” alisema Zitto wakati akihutubia umati mkubwa wa watu katika uwanja wa Magereza.

Pamoja na mambo mengine, Zitto alisema haogopi kushindwa kwenye uchaguzi iwapo ataamua kugombea ubunge katika jimbo jingine na kwamba dhamira yake ya kutaka kugombea nje ya jimbo lake ni kukuza na kuchochea maendeleo.

Aidha, Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma, alisema serikali ya Tanzania inapoteza zaidi ya sh bilioni 27 kila mwaka kutokana na kushindwa kupeleka umeme katika baadhi ya migodi nchini.

Alisema serikali imekuwa ikilipwa sh milioni 230 za mirahaba ya migodi kwa mwaka fedha ambazo ni kidogo mno.

Kuhusu upotevu wa mamilioni hayo, alisema migodi imekuwa ikizalisha umeme wao, jambo ambalo serikali imeshindwa kulipatia ufumbuzi kwa kupeleka huduma hiyo.

“Wamiliki wa migodi wanatumia sh bilioni 27 kwa mwaka kuzalisha umeme migodini mwao badala ya serikali kupeleka umeme huo,” alisema Zitto.

Kuhusu fedha za mirahaba, alisema wilaya zenye migodi kama Geita zimekuwa zikilipwa sh 200,000 kwa mwaka, fedha ambazo alisema haziendani na uzalishaji wake.

Akisisitiza juu ya hilo, alisema Kamati ya Bomani imependekeza kiasi hicho kifikie sh bilioni 4 mwaka kwa malipo hayo ya mirahaba.

Wakati Zitto akiwasha moto Geita, Mbunge wa Moshi Mjini ameibeza harambee ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kilimanjaro ya kukusanya sh milioni 500 kwa ajili ya kampeni za kulinyakua jimbo hilo katika uchaguzi mkuu ujao.

Ndesamburo amekuwa mbunge wa jimbo hilo tangu mwaka 2000 na amekuwa mwiba mkali kwa CCM ambapo mara mbili mfululizo alimshinda mpinzani wake, Elizabet Minde wa CCM.

Akizungumza na Tanzania Daima mwishoni mwa wiki mjini hapa, Ndesamburo maarufu kwa jina la 'Ndesa Pesa' alisema hata siku moja chama hicho kisitarajie kulinyakua jimbo hilo kwa kuendesha kampeni za kuwahonga wananchi.

Alikitaka chama hicho kisiishie kupata sh milioni 500 pekee bali kiende mbali hata ikiwezekana kikusanye sh bilioni moja, ili wananchi wa jimbo la Moshi Mjini waneemeke na fedha hizo ambazo amedai ni jasho lao.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Vicky Nsilo Swai, alilithibitishia Tanzania Daima kuwa harambee hiyo itafanyika Mei na itaongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho, Rais Jakaya Kikwete.

Harambee hiyo ni sehemu ya mikakati ya CCM mkoani hapa kujiimarisha kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu na hivi karibuni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitoa sh milioni tano kwa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Manispaa ya Moshi kwa ajili ya kambi ya vijana hao yenye lengo la kujiweka sawa na uchaguzi huo.

Katika uchaguzi mkuu mwaka 2005, CCM Mkoa wa Kilimanjaro ilikusanya sh milioni 200 kwa ajili ya kufanikisha kampeni za uchaguzi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha jimbo hilo linanyakuliwa na chama hicho lakini haikuwezekana.

Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kazidi, kwa wiki nzima sasa amekataa kuzungumzia harambee hiyo kwa kile alichodai hayo ni masuala ya ndani ya chama hicho na kuongeza kuwa wakati ukifika wataiweka wazi hata kwenye vyombo vya habari.

No comments: