Tuesday, February 16, 2010

TRL kwawaka moto

• Wafanyakazi watishia kugoma

na Sauli GiliardAHADI ya serikali ya kuwalipa mishahara wafanyakazi wa Kampuni ya Reli (TRL) imeshindwa kutekelezeka.

Wiki iliyopita, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU), Sylvester Rwegasira aliwatangazia wafanyakazi kuwa hundi ya malipo yao ingekuwa tayari hadi kufikia jana, lakini kinyume na matarajio yao, watendaji wa Wizara ya Miundombinu walikuwa bado hawajafikia muafaka.

Tanzania Daima ilipomtafuta katibu huyo kueleza iwapo madai hayo yamefanyiwa kazi, alisema hadi jana mchana wakati anaondoka katika ofisi ya Mkurugenzi wa Usafirishaji wa wizara hiyo hakukuwepo dalili yoyote ya hundi ya malipo kutolewa.

“Ndiyo naondoka...natoka kikaoni na mkurugenzi wa wizara, ile ahadi haitekelezeki, leo ndiyo naenda kuwaeleza wafanyakazi watajua nini cha kufanya. Siwaambii la kufanya, wao wanajua watafanya nini,” alisema Rwegasira.

Kwa mujibu wa Rwegasira, hundi ambayo aliifuatilia wizarani ni ya thamani ya sh milioni 900 na kuongeza kwamba malipo hayo yamebaki baada ya kutolewa malipo ya sh milioni 800.

Katika maelezo yake wiki iliyopita, Rwegasira alibainisha iwapo tamko hilo la Katibu Mkuu kwa wafanyakazi hao kupewa stahiki ya mishahara, wangeitisha mgomo ili kuishinikiza serikali kutekeleza ahadi hiyo.

Alieleza lengo jingine lilikuwa ni kuishinikiza serikali ivunje mkataba wake na Kampuni ya Rites ambayo serikali imeingia nayo ubia ili kuiendesha Kampuni ya TRL.

Rwegesira alilidokeza gazeti hili kuwa jana kulikuwa na mkutano mrefu ulioanza majira ya asubuhi katika ofisi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Mhandisi Omari Chambo juu ya ulipwaji wa mishahara hiyo, lakini hadi mchana hakukuwepo dalili zozote za kufikia muafaka.

“Ofisini kwa katibu mkuu kulikuwa na kikao cha muda mrefu tangu asubuhi juu ya malipo ya wafanyakazi wa TRL, hadi sasa hakuna muafaka uliofikiwa ndugu yangu,” alisisitiza.

Alisema hundi hiyo ambayo Chambo amemwambia iko tayari, ilipaswa kutolewa jana, lakini ahadi hiyo haikutekelezwa.

“Katibu mkuu amesema hundi iko tayari na itatolewa leo (jana), lakini hawajaitoa, tutaitisha maandamano kuiomba serikali ivunje mikataba na sisi, kwani tunaona uwezekano wa kuvunja mikataba na wawekezaji imeshindikana,” alisema Rwegasira.

Katika ubia huo wa kuiendesha TRL, serikali inamiliki hisa asilimia 49 wakati Rites inamiliki asilimia 51 na kuwa na sifa ya kuunda menejimenti ya kampuni huyo.

No comments: