Wednesday, February 24, 2010

Spika Sitta, hiyo si kinga

Irene Mark
KWA mara kadhaa, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, amenukuliwa na vyombo vya habari akitumia jina la Mungu na maandiko matakatifu kama silaha na ndiko anakopata ulinzi wake.

Awali nilimsikia Sitta akisema neno linalompa nguvu na ujasiri linatoka kwenye kitabu cha Ayubu sura ya 19 mstari wa 25 usemao: “Najua ya kuwa mtetezi wangu yu hai na najua ya kuwa atasimama juu yangu.”

Kwa kauli zake, maneno hayo ndiyo yanayomfariji na kumwongezea ujasiri pindi anapokutana na vikwazo, hasa katika utendaji wa shughuli zake bungeni.

Nimewahi kumsikia akieleza kwamba wakati unaompa shida kwenye kuendesha vikao vya Bunge ni katika kujadili suala la Richmond na mapambano dhidi ya ufisadi.

Kwangu, Sitta ni mwanasiasa sawa na wengine. Sishangazwi wala kushtushwa na maneno yake, nikikumbuka mwanzo wa safari ya utawala wa nne na tafsiri tofauti ninazozipata akilini mwangu, ndiyo msingi wa makala hii.

Baada ya kushindwa kwenye kura za maoni kwa ajili ya kumpata mgombea urais kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1995 kwa kile kilichoitwa ‘zengwe’ la Mwalimu Nyerere, Jakaya Kikwete alijipanga ili kuhakikisha mwaka 2005 kura zinatosha kumteua.

Moja ya mipango yake ni kuingia kwenye nyumba za ibada. Alianzia kanisani. Ulipokaribia uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 maaskofu, mapadri na watumishi wakatengeneza mbegu hafifu na kuwalisha waamini wao kwamba Kikwete ni chaguo la Mungu.

Neno likawaingia waamini. Mbegu hafifu ikamea kwa muda kuwa hakuna zaidi ya Kikwete kwa sababu viongozi wa dini wamesema ndilo chaguo la Mungu. Watanzania walio wengi wakaamini na kumwona ndiye mgombea pekee.

Mzizi ukashika ardhi kwamba chaguo la watu ni chaguo la Mungu. Ikaenea, ikakubalika hivyo kwa sababu hata wasiomfahamu walilazimishwa kuamini kuwa mgombea urais wa CCM ndilo chaguo la Watanzania wote.

Ilifika pahala ukimuuliza shabiki wa Kikwete aeleze alichokifanya kikaonekana na mgombea huyo kwa masilahi ya taifa ni kipi, huwezi kupata jibu. Badala yake likaongezeka neno ‘ana mvuto wa kisiasa’.

Kana kwamba haitoshi, miaka miwili baadaye baadhi ya viongozi wa dini wakachoshwa na mwenendo wa nchi. Mbegu ya chaguo la Mungu ikafa rasmi, hakuna aliyesikika akihubiri neno hilo tena.

Wananchi wakaanza kulalamika na kuukumbuka utawala wa Awamu ya Tatu kwa sababu kila kunapokucha afadhali ya jana.

Wachache tulioletewa chaguo la Mungu (ile asilimia 20 ambayo hatukumpigia kura Kikwete), tulikosa maneno ya kusema mbele ya wengi, tukaungana nao katika vifo vilivyosababishwa na njaa, tatizo la umeme lililosababisha Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kuvunja Baraza la Mawaziri pale alipojiuzulu, akifuatiwa na mawaziri wengine wawili.

Pamoja na hayo, tumeshuhudia mauaji ya albino, ugumu wa maisha, kimbizakimbiza ya wamachinga na mambo mengine. Kutokana na hayo nikaamini kuwa adhabu tunazozipata zinatokana na dhambi ya kumsingizia Mungu kwamba Kikwete ni chaguo lake.

Ni hivi karibuni ambapo Askofu Anthony Lusekelo, maarufu kwa jina la ‘Mzee wa Upako’, aliwakebehi wanasiasa wanaokimbilia makanisani kuwa wamefilisika kisiasa.

Mzee wa Upako anamaanisha anachokisema. Kwa tafsiri nyingine anakiri dhambi iliyofanywa na viongozi wenzake wa dini, ambapo mzigo mkubwa sasa unawaangukia waamini wao.

Msingi katika mtazamo wangu ni kumweleza Spika Sitta kwamba kulifahamu neno la Mungu si kinga, bali kuliishi na kulitenda ndiyo silaha bora katika ulinzi wa kila siku.

Ninachoamini katika ngoma ya siasa hakuna mkweli. Ndiyo maana napata ukakasi juu ya kauli za Spika huyu ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), kwa sababu ametajwa kuwamo katika makundi ndani ya chama chake.

Hapa nakosa pa kumweka Spika Sitta kwa sababu anatumia kanisa kama ilivyokuwa kwa Kikwete miaka mitano iliyopita, hali inayoweka kivuli kwa wapiga kura wa Urambo Mashariki kujua yanayomhusu nyuma ya pazia ili kufanya uamuzi sahihi kwenye uchaguzi ujao.

Nalazimika kuamini kuwa Sitta amegeuza mistari mitakatifu kuwa kichaka chake, ilhali zipo taarifa kwamba amegomea suluhu kati yake na aliyekuwa Waziri Mkuu, Lowassa na kuilazimisha Kamati maalumu inayoongozwa na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, yenye kazi ya kuondoa makundi ndani ya wabunge wa CCM kuongezewa muda.

Si kawaida yangu kumaliza bila kutoa ushauri na huu umfikie Sitta, namuomba apatane kwanza na mahasimu wake ili kuiaminisha jamii kwamba anaishi na kulitenda neno.

Biblia inasema, visasi ni vyake Mungu, pia inatusihi kutokuwa na maadui na hata tukiwa nao tuwapende na kuwaombea maisha marefu. Spika, usipofanya hivi, utanizidishia maswali magumu kichwani mwangu.

No comments: