Thursday, February 25, 2010

CHADEMA yaitisha maandamano Musoma

na Mabere Makubi, Musoma
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Mara kimepanga kufanya maandamano makubwa ya kuingia ndani ya mgodi wa dhahabu wa North Mara, wilayani Tarime kudai asilimia moja ya vijiji vitano vinavyouzunguka kulingana na mkataba na mwekezaji.

Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mara, Machage Bartholomew Machage alisema kwenye mkutano wa hadhara kuwa zaidi ya miaka 10 ya uchimbaji wa dhahabu katika mgodi huo, vijiji vitano vya Kewanja, Kerende, Nyamwaga, Genkuru na Nyangoto havijawahi kulipwa asilimia moja ya mapato ya mgodi huo kama ilivyo kwenye mkataba.

Machage alisema mwekezaji huyo pia ameshindwa kutekeleza huduma za jamii alizoahidi kuzitoa katika vijiji hivyo, ambazo ni ujenzi wa vituo vya afya, umeme, maji, barabara na shule, badala yake amekuwa akifanya ukarabati kinyume cha mkataba aliowekeana na serikali za vijiji hivyo.

“Tutaitisha maandamano makubwa ya wananchi, na mimi ndiye nitakayeyaongoza kuelekea mgodini ili tuishinikize serikali iweze kumwagiza mwekezaji atoe asilimia moja ya mapato yake. Wananchi wa Nyamongo hatuwezi kuendelea kubaki masikini wakati dhahabu yetu inawanufaisha watu wengine, nipeni muda nimalize ziara zangu, halafu nitakuja tufanye maandamano,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Vijana wa CHADEMA Wilaya ya Musoma Mjini, Mwita Julius alisema licha ya Mkoa wa Mara kuchangia pato la taifa kwa zaidi ya asilimia 10 kutokana na dhahabu inayochimbwa kwenye mgodi wa North Mara, inasikitisha kuona kwamba wakazi wa Nyamongo wanaishi katika lindi la umasikini.

Mkutano huo wa hadhara ni wa kwanza kuhutubiwa na Machage tangu alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mara kujaza nafasi iliyoachwa wazi na marehemu Chacha Wangwe aliyefariki dunia mwaka juzi.

No comments: