Thursday, February 25, 2010

CCJ yasajiliwa

na Irene Mark
HATIMAYE Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imeridhia kukipa usajili wa muda Chama Cha Jamii (CCJ), baada ya kukikwepa kwa zaidi ya miezi miwili.

Habari za uhakika zilizoifikia Tanzania Daima zinasema ofisi ya msajili jana ilimwandikia mwenyekiti wa muda wa CCJ, Richard Kiyabo yenye kumbukumbu namba RPP/CCJ/136/09, ikijibu maombi ya usajili wa muda.

Barua hiyo iliyoandikwa na Ibrahim Mkwawa kwa niaba ya msajili, ilisema itakikabidhi chama hicho cheti cha usajili wa muda Machi 2 mwaka huu saa tano asubuhi katika ofisi za msajili.

Ilieleza kuwa msajili ameridhika na maombi ya usajili wa muda wa chama hicho baada ya kukidhi matakwa ya sheria namba tano ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 na Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

“Hivyo basi, Msajili wa Vyama vya Siasa atakabidhi cheti cha usajili wa muda kwenu siku ya tarehe 2/03/2010 saa tano asubuhi kwenye ofisi ya msajili,” ilieleza sehemu ya barua hiyo ambayo Tanzania Daima ilipata nakala yake.

Licha ya kupatikana kwa barua hiyo, ofisi ya msajili imetaka kuongezewa nakala tatu za katiba ya chama hicho kabla ya kukabidhiwa rasmi cheti cha usajili wa muda mapema juma lijalo.

Jana, gazeti hili liliandika kuhusu ucheleweshwaji wa usajili wa muda hali iliyodaiwa kukwamisha utekelezaji wa baadhi ya mambo kwa lengo la kujiimarisha kama chama ili kukabiliana vilivyo kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Hata hivyo, ofisi ya msajili iliahidi kukutana na CCJ leo ili kuwapa maelekezo ya lini hasa watapata usajili wa muda, lakini katika hali ya kushtukiza, viongozi wa chama hicho walipokea simu zilizowataka kufika ofisini kwa msajili jana mchana.

“Tumepokea simu kutoka kwa msajili mwenyewe akisema kwa nini tumeamua kumshitaki kwa jamii, sasa ametuita… sijui anakwenda kuzungumza nini, tukishakutana nae mchana wa leo (jana) tutajua cha kufanya,” kilieleza chanzo cha habari chenye kuaminika kutoka CCJ na kuongeza kwamba, ahadi ya kukutana na msajili ilikuwa leo.

Awali, viongozi wa juu wa chama hicho walisema tayari chama chao kimetengeneza katiba, kanuni za chama, bendera, kadi na kwamba inao zaidi ya wanachama 3,000 kwa Dar es Salaam pekee, hivyo walikuwa wakisubiri kupata usajili kabla ya kukizindua rasmi.

Sehemu ya Katiba ya CCJ inaeleza: “Kwa kuwa Tanzania inao utajiri wa kutosha wa rasilimali unaoweza kuleta maendeleo ya haraka ya nchi kiuchumi na kuleta mabadiliko makubwa ya maisha kwa kila mwananchi ikiwa ombwe la uongozi litashughulikiwa.”

Sehemu nyingine ya katiba hiyo inaeleza kwamba itahakikisha utajiri wa rasilimali zilizopo unatumika kwa maendeleo ya wananchi kwa kuondoa umaskini, ujinga, na maradhi huku aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, uonevu, rushwa au ufisadi vinatokomezwa nchini.

Ujio wa CCJ umeleta mtikisiko ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na kutajwa kuhusisha vigogo wa chama hicho tawala ambao wanataka kujitenga na kugombea urais Oktoba mwaka huu.

Hata hivyo, baadhi ya wadadisi wanadai kuanzishwa kwa CCJ ni mkakati wa Idara ya Usalama wa Taifa, ambayo ina lengo la kupotosha umma kuhusu hatima ya CCM na Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Vile vile, wanadai CCJ imeanzishwa ili kuupotosha umma unaoikosoa CCM, na kuumaliza nguvu upinzani, hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho kimekuwa mwiba mkali kwa CCM katika miaka ya hivi karibuni.

Baadhi ya vigogo wa CCM wanaohusishwa na CCJ ni Spika wa Bunge Samuel Sitta, makundi ya wanachama na viongozi waliojiweka mbele kupambana na ufisadi, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba na John Malecela. Lakini wote wamekanusha jambo hilo.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa, hatua ya vigogo hao kuikana CCJ ni mwanzo mbaya na fursa iliyopotea ya kukikuza na kukijenga chama hicho.

Wapo baadhi ya vigogo waliojitambulisha na chama hicho, lakini hawataki kutajwa majina magazetini kwa sasa.

No comments: