Monday, April 27, 2009

Simba SC uuuh!


Timu soka ya Simba ya Dar es Salaam jana ilijihakikishia kucheza michuano ya kimataifa mwakani, baada ya kuifunga Polisi Dodoma mabao 2-0 katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.

Matokeo hayo yamewafanya mashabiki wa Simba kupumua, kutokana na kutokuwa na raha kwa kukosa michuano ya kimataifa inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa mwaka huu, hivyo jana walikuwa wakisubiri kwa hamu kubwa matokeo ya mchezo huo. Simba iliyoingia uwanjani ikiwa na pointi 37 ilikuwa ikihitaji ushindi ili ijihakikishie 'kupanda ndege' mwakani katika michuano ya kimataifa, ambapo kinyume na matokeo hayo ingejiweka pabaya, kwani Mtibwa Sugar iliyokuwa na pointi 35 nayo jana ilicheza na Polisi Morogoro na kushinda mabao 3-2.

Simba sasa imefikisha pointi 40, wakati Mtibwa ina pointi 38. Mabao ya Simba yalifungwa na Haruna Moshi dakika ya 69, kisha Mohammed Kijuso alifunga bao la pili dakika ya 81, Beki Said Gabeza alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 72 kutokana na mchezo mbaya. Kutoka Mbeya, Merali Chawe anaripoti kuwa Moro United jana iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. Moro United ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya tisa mfungaji akiwa Thomas Mourice baada ya kupokea pasi ya Amri Kiemba.

Prisons ilisawazisha bao hilo dakika ya 40 mfungaji akiwa Fred Chudu, baada ya kipa Haji Macharazi wa Moro kuutema mpira na kumkuta mfungaji. Moro United ilipata bao la pili dakika ya 68, baada ya beki David Mwantike kujifunga kwa kichwa katika harakati za kuokoa, ambapo matokeo hayo yameifanya Moro United ifikishe pointi 25. Matokeo hayo yanaipa nafasi Moro United kubaki katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao, badala yake Polisi Moro inashuka daraja kutokana na kufungwa mabao 3-2 na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Timu zote hizo zina pointi 25, ambapo ukiangalia uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa zote ni 0-0, ambapo Moro United imefunga mabao 31 na imefungwa 31, wakati Polisi Moro imefunga mabao 25 na imefungwa 25. Kulingana na kanuni za ligi hiyo zilizotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kama timu zitafungana pointi itatazamwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa, lakini pia kama zitafungana itaangaliwa timu yenye mabao mengi ya kufunga, ambapo kwa timu hizo mbili ni Moro United yenye mabao 31 ukilinganisha na 25 ya Polisi.

"Ikiwa timu mbili zitalingana kwa pointi baada ya michezo mshindi atapatikana kwa tofauti bora ya magoli ya kufungwa na kufunga, kama tofauti hiyo haitoi mshindi, mshindi atakuwa ni mwenye magoli mengi ya kufunga, kama pia magoli ya kufunga hayatoi mshindi, basi mshindi atakuwa ni yule atakayekuwa na pointi nyingi kwenye michezo miwili iliyohusisha timu hizi mbili.

“Na kama pia michezo hiyo haitoi mshindi, mshindi atakuwa yule aliyefunga magoli mengi zaidi katika mchezo wa ugenini uliozihusisha timu hizi mbili, iwapo bado haitoi mshindi, mshindi atakuwa aliyefunga magoli mengi ya ugenini katika msimu mzima, iwapo bado haitoi mshindi timu hizi zitacheza mchezo mmoja katika uwanja utakaochaguliwa na TFF, na taratibu zote za kupata mshindi zitafuatwa kama mchezo wa fainali, " inasema kanuni ya sita ya ligi kuhusiana na mshindi.

Kwa mujibu wa Mwandishi John Nditi, mabao ya Mtibwa yalifungwa na Said Mkopi dakika ya pili, kabla ya Ally Moshi kusawazisha dakika ya tatu, kisha Soud Abdallah wa Mtibwa kufunga la pili dakika ya 16, Polisi ikasawazisha dakika ya 17 mfungaji akiwa Fred Hagai. Bao la ushindi la Mtibwa lilifungwa dakika ya 44 na Shaaban Nditi. Kutoka Mwanza, Toto African iliifunga Azam FC bao 1-0, lililofungwa dakika ya 51 na Hussein Sued, matokeo ambayo yameifanya Toto ifikishe pointi 28 hivyo kuepuka kushuka daraja.

Naye Mwandishi Wetu anaripoti kuwa mchezo kati ya Yanga na Villa Squad uliokuwa ufanyike jana ulikwama kutokana na mvua kubwa iliyonyesha, hivyo Uwanja wa Uhuru kujaa maji. Kutokana na michezo hiyo ya mwisho ya ligi jana, Polisi Moro sasa inaungana na Polisi Dodoma yenye pointi 18 na Villa Squad yenye pointi 15 kushuka daraja, ambapo mwakani zitacheza ligi daraja la kwanza.Yanga ndiyo bingwa wa ligi hiyo, wakati Simba imeshika nafasi ya pili.

No comments: