Tuesday, April 28, 2009

Muungano waibua malumbano makali katika televisheni ya taifa

Na Salim Said

MVUTANO mkali umeibuka miongoni mwa wasomi, wanasiasa na serikali katika mjadala kuhusu kero za Muungano uliofanyika jijini Dar es Salaam juzi.


Katika mjadala huo, baadhi ya washiriki walikua wakinyoosheana vidole na kutuhumiana kuwa, ndio wanaosababisha kukua na usugu wa kero za Muungano wa Tangayika na Zanzibar.


Mjadala huo ambao ulirushwa na Kituo cha Televesheni TBC1 uliwashirikisha baadhi ya wasomi, viongozi wa serikali na wanasiasa..


Waziri wa Nchi katika ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Muhmmad Seif Khatib alisema muungano umeimarika na kwamba ndoto za waasisi wake, ambao ni mwalimu Julius Nyerere na hayati Abeid Aman Karume zimetimia.


Kauli hiyo pia, iliungwa mkono na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azaveli Lwaitama ambaye alisema muungano umeimarika na kwamba, falsafa ya waasisi imetimia.


“Hata ukimuuliza ndugu yangu Duni hapo, atakwambia yeye ni Mtanzania, kero zinakuzwa na wanasiasa ambao hawajaelewa, yaliyokuwamo katika vichwa vya waasisi wa muungano huu” alisema Dk Lwaitama


Kauli hizo zilionyesha kumkera Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Juma Duni Haji ambaye katika kujibu hoja hiyo alisema, “kama kuimarika kwa muungano ni kuwepo kwa kero nyingi na matatizo, basi umeimarika lakini kama ni utatuzi wa matatizo na kero hizo, basi bado haujaimarika”.


“Katika mambo ambayo siyapendi na yananikera sana ni kuufananisha muungano huu kuwa ni wa mke na mume au mkubwa na mdogo. Huu ni muungano wa nchi mbili. Mimi nikiwa Katibu wa Wizara ya Fedha tuliisaidia serikali ya muungano dola 15 milioni za Marekani kulipa deni la Benki ya Dunia,” alisisitiza Duni.


Jambo hilo, lilimfanya muongoza mjadala huo ambaye ni mtangazaji wa TBC1, kumuomba radhi mwanasiasa huyo na kuruhusu mjadala huo kuendelea.


Duni aliendelea kutoa mifano ya kutoimarika kwa muungano huo kuwa, ni pamoja na kufukuzwa katika chama, kwa Rais mstaafu, Aboud Jumbe na maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alikuwa waziri kiongozi wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kutoka na kesi za muungano.


“Muungano lazima ulete faida kwa wananchi kisiasa, kiusalama na kiuchumi lakini Wazanzibari wanahoji kuhusu fedha za misaada na mikopo zinazoingia nchini kwa jina la Tanzania, kwa nini hawapati,” alihoji Duni


Alisema, jambo muhimu ni kushughulikia kero za muungano na si kuwa, mtu akisema aitwe katika vikao vya kamati kuu ya chama na kunyamazishwa au kuadhibiwa.


Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari, Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (Misa- Tan), Ayoub Rioba alisema, kama kuna mawasiliano yanayoeleweka, baina ya viongozi na wananchi, matatizo ya kero za muungano yatamalizika.


“Kama tutakuwa na mawasiliano imara baina ya pande mbili hizi, tatizo ni dogo sana lakini pia tuthamini michango ya mijadala kama hii, kwa kuwa bado sisi tunayo fursa ya kujadiliana, wenzetu wanatafuta lakini hawapati fursa ya kujadiliana” alisena Rioba.


Katika hilo, Dk Lwaitama alisistiza kuwa, dhamira ya waasisi ilikuwa ni umoja na mshikamano wa Watanzania na Waafrika lakini matatizo na kero ni jambo la kawaida.


Kwa upande wake waziri Khatibu alisisitiza kuwa, uhuru, usalama, amani na uchumi wa Zanzibar unategemea serikali ya muungano iliyopatikana baada ya kuungana kwa Zanzibar na Tanganyika mwaka 1964.


“Muungano ni wa binadamu wala si wa malaika, matatizo hayaepukiki lakini tunafanya jitihada mbalimbali za kutatua kero na matatizo hayo” alisema Khatib.

No comments: