Sunday, December 7, 2008

Hii ni hatari

• Wanaotaka kumuondolea kinga Mkapa kukiona


na Mwandishi Wetu
TANZANIA hivi sasa inaelekea katika kipindi kigumu zaidi kisiasa, kiuchumi na kijamii kutokana na kuibuka kwa makundi ndani na nje ya serikali yenye mitazamo tofauti na hatarishi juu ya mustakabali wa nchi.

Tofauti ya makundi hayo sasa imegeuka uadui na kutishiana maisha, na kuhatarisha mwelekeo wa kisiasa na kijamii, kwa kila kundi likidai kundi jingine linafanya kazi kwa kuhatarisha masilahi ya jingine.

Mwelekeo wa siasa hasa uchaguzi wa mwaka 2010 unaaanza kumezwa na nguvu na ushawishi wa fedha wa moja ya makundi hayo ambalo limedhamiria kutumia fedha ili wote wanaokemea ufisadi, wasiweze kupata nafasi za kisiasa.

Inadaiwa kuwa kundi hili, linapita katika baadhi ya majimbo ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao wamejitolea kupigana vita dhidi ya ufisadi, wakiwaandaa watu wao wanaowataka ili wachukue majimbo hayo na kutetea maslahi yao bungeni na serikalini.

Kundi hilo pia linadaiwa kuupa wakati mgumu utawala wa Rais Jakaya Kikwete ambao katika siku za hivi karibuni, umekumbana na vikwazo kadhaa vikiwemo vya migomo ya walimu, wafanyakazi TRL na wanafunzi wa vyuo na taasisi za elimu ya juu, wote wakitoa madai mbalimbali yanayohusu kutolipwa stahiki zao.

Wakati kundi hilo likijizatiti hivyo, kundi jingine nalo limeimarisha ngome yake kuhakikisha wote waliohusika katika ufisadi, wanawajibishwa bila kujali nafasi au heshima waliyonayo mbele ya jamii.

Kundi hili linapata wakati mgumu kutokana na baadhi ya watu wanaowasaidia wanaotuhumiwa kwa ufisadi kuwa na uwezo wa kifedha pamoja na ushawishi ndani na nje ya serikali huku wengine wakiwa ni viongozi wa serikali.

Wakati hali ya mambo ikiwa si shwari kwa makundi hayo mawili, kuna baadhi ya wabunge hivi sasa inadaiwa wameandaliwa mkakati wa kushughulikiwa ili wasishinde katika uchaguzi mkuu ujao, baada ya kuonyesha nia ya kutaka kuwasilisha hoja binafsi kutaka Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa aondolewe kinga na kushitakiwa.

Wabunge hao (majina tunayahifadhi), walionyesha kukerwa na kitendo cha serikali cha kuwafikisha mahakamani mawaziri wa zamani, Daniel Yona (Nishati na Madini) na Basil Mramba (Fedha), kwa matumizi mabaya ya madaraka yao ilhali Benjamin Mkapa akiendelea na kazi zake kama kawaida.

Walibainisha wazi kuwa si haki wala busara kwa Yona na Mramba pekee kuburuzwa kortini kwa matumizi mabovu ilhali upo msusuru mkubwa wa viongozi waliopo madarakani na waliomaliza muda wao waliotumia vibaya madaraka yao kwa kuliingiza taifa kwenye hasara ambazo hazijabainishwa.

“Tumeshapokea barua za maonyo na vitisho kuwa mchakato tunaotaka kuufanya utatugharimu na kuna kila dalili za kutoweza kurudi katika ubunge, hatuogopi kwani tuna imani tunasimamia haki,” alisema mmoja wa wabunge hao.

Wakati wabunge wakifikiria kupeleka hoja binafsi ya kumuondolea kinga Mkapa, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alishaweka bayana kuwa jambo hilo linaruhuriwa ila linahitaji uungwaji mkono wa theluthi mbili ya wabunge.

Mambo hayo ya viongozi wa siasa yakiwa bado moto, hivi sasa kumezuka malumbano ya maneno baina ya mfanyabiashara maarufu na Mwenyekiti wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Lawrence Masha, kuhusu kuhujumiwa kwa mfanyabiashara huyo pamoja na kutishiwa kuuawa.

Mengi wiki iliyopita alidai kuwa anapokea ujumbe wa kutishiwa kuuawa pamoja na kupata taarifa za kutaka kuhujumiwa kibiashara na mmoja wa mawaziri vijana wa Serikali ya Awamu ya Nne.

Kwa mujibu taarifa za vitisho hivyo kulikuwa na kikao cha siri cha usalama ambacho kilimuona Mengi kama mmoja wa watu wanaoyumbisha utawala huu, hasa kutokana na kelele zake za kukemea ufisadi, hivyo njia pekee ya kumzima ni kumhujumu katika biashara zake.

Masha naye juzi katoa siku saba kwa Mengi kumtaja waziri huyo na kuthibitisha madai ya kutaka kuhujumiwa, la sivyo atakumbana na mkono wa sheria.

Vitisho na kauli hizi zinaonekana kuwa na athari kwa namna moja au nyingine kwani baaadhi ya Watanzania hivi sasa wameshagawanyika katika pande mbili huku wengine wakimuunga mkono Mengi na wengine wakimuunga mkono Waziri Masha.

Hali hii ni hatari kwa mustakabali wa taifa kwa siku za usoni, hasa uchaguzi mkuu ujao ambao umeshaanza kuonyesha nyufa baina ya watu na watu.

Umoja, amani na utulivu miongoni mwa jamii vilivyokuwa vikihimizwa na Baba wa Taifa hayati Julius Nyerere hivi sasa vinaelekea kukosa nguvu, baada ya baadhi ya watu, hasa viongozi kushindwa kuwaunganisha watu na kusuluhisha migogoro midogo midogo inayoanza kuchipuka hivi sasa.

No comments: